Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 50 kutoka CERF zatengwa kuisaidia Syria:

Dola milioni 50 kutoka CERF zatengwa kuisaidia Syria:

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura Bi Valerie Amos, leo ametenga dola milioni 50 kutoka kwenye mfuko wa Umoja wa Maraifa wa dharura CERF ili kupiga jeki juhudi za mashirika ya misaada ya kibinadamu yanayosaidia idadi inayoongezeka ya Wasyria walioathirika na vita vinavyoendelea ndani ya nchi na katika kanda nzima.

Bi Amos amesema hali ya Wasyria wanaokimbia vita nchini mwao inazidi kuwa mbaya kila kukicha na ndio maana ametoa fedha hizo kuyasaidia mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa ili kuongeza kazi zao kuweza kukabiliana na mahitaji yaliyopo, na mchango huo wa CERF unaonyesha mshikamano kwa watu wa Syria kwani fedha hizo zinatoka kwa wahisani , wakubwa na wadogo kote duniani.

Fungu la leo la CERF ni kubwa kabisa kuwahi kutolewa mara moja kusaidia katika mgogoro mmoja. Kati ya fedha hizo dola milioni 20 zitasaidia operesheni za misaada ndani ya Syria, dola milioni 15 zitakwenda kusaidia juhudi za misaada Lebanon, dola milioni 10 zitasaidia wimbi la wakimbizi wa Syria Iraq na dola milioni 5 zilizosalia zitasaidia misaada ya kibinadamu Jordan.

Idadi ya Wasyria walioathirika na vita imeongezeka haraka huku watu milioni 4.2 wakiwa wakimbizi wa ndani na wengine milioni 2 wamekimbilia katika nchi jirani. Mipango ya kukabiliana na matatizo ya kibinadamu Syria hadi sasa imepokea nusu tuu ya dola bilioni 4.4 zinazohitajika.

Kabla ya msaada wa leo wa CERF nchi nyingine pekee ambayo iliwahi kupokea kiwango kikubwa cha fungu la msaada ni Somalia mwaka 2010 ambapo mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo ulipewa dola milioni 30 kukabili athari za ukame na upungufu wa chakula.