Vikosi vya serikali Syria vyalaumiwa kushambulia hospitali

13 Septemba 2013

Tume huru ya kuchunguza Syria imesema kumekuwepo na ongezeko kubwa la matukio yanayowalenga watumishi wa huduma za kijamii ikiwemo hospitali, watabibu pamoja na mifumo ya usafiri. Katika ripoti yake tume hiyo imeeleza kuwa kukithiri kwa matukio hayo kunazorotesha ustawi wa taifa hilo ambalo bado linakabiliwa na mapigano baina ya vikosi vya serikali na makundi ya waasi.

Ripoti hiyo imelaumu pande zote za mapigano ikisema kuwa mienendo yao inanyima fursa wananchi kupata huduma za matibabu. Tume hiyo imesema kuwa kumekuwepo pia matukio yanayofanywa na wafuasi wa serikali na vikundi vya waasi ambao kwa nyakati tofauti hushambulia kwa makusudi hospitali na vituo vya huduma ya kwanza.