Rais Bashar Al Assad asaini nyaraka za kujiunga na mkataba unaozuia silaha za kemikali

12 Septemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon Alhamisi amepokea barua kutoka serikali ya Syria inayomtaarifu kuwa Rais Bashar Al Assad ametia saini nyaraka za kuwezesha nchi hiyo kujiunga na mkataba wa kimataifa wa kupiga marufuku uendelezaji, utengenezaji, uhifadhi na utumiaji wa silaha za kemikali wa mwaka 1992.  Msemaji wa Katibu Mkuu katika taarifa yake ameeleza kuwa kwenye barua hiyo serikali ya Syria imeeleza utayari wake wa kuwajibika kwa mujibu wa mkataba huo kabla hata kabla ya kuridhia. Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesifu hatua hiyo na kueleza kuwa yeye akiwa msimamizi wa mkataba huo kwa muda mrefu amekuwa akitaka nchi zote kuridhia mkataba huo . Bwana Ban amesema kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni, ni matumaini yake kuwa mazungumzo ya Geneva yatachochea mwelekeo wa baadaye ambao utaridhiwa na kupata usaidizi wa jumuiya ya kimataifa.