Dunia yaweza kuepuka gharama za bilioni 47 na kuokoa zingine kwa uwekezaji wa Global Fund

12 Septemba 2013

Ripoti mpya iliyotolewa Alhamisi iitwayo “Gharama za bila kuchukua hatua” inatoa changamoto kwa viongozi wa dunia kutunisha mfuko wa kimataifa kwa ajili ya kupambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria yaani Global Fund. Flora Nducha na taarifa kamili

 (TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Maafisa wa Global Fund wamepiga mahesabu na kusema zinahitajika dola Bilioni 15 katika miaka mitatu ijayo ili kuanza kudhibiti maradhi hayo matatu yanayoisumbua dunia.  Miongoni mwa mambo yaliyobainiwa na ripoti hiyo ni kwamba endapo ufadhili hautopatikana kutakuwa na visa vipya Milioni 2.6 vya maambukizi ya HIV kila mwaka ambapo visa Milioni 1.3 kati ya hivyo vingeweza kuepukika.

Kwa upande wa kifua kikuu watu Milioni Tatu watakosa tiba na kati yaoMilioni Moja kupoteza maisha  pasi kustahili, huku malaria athari zake zitasababisha kukatikli maisha ya watu 196,000 kila mwaka na wengine milioni 430 kuugua hali ambayo ingeweza kuzuilika.