Matumzi mabaya ya chakula husababisha athari kwa mazingira na hali ya hewa: FAO

11 Septemba 2013

Shirika la kilimo na chakula duniani, FAO kwa ushirikiano na Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP hii leo yamezindua ripoti inayoonyesha jinsi matumzi mabaya ya chakula yanaweza kusababisha athari kwa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa. Alice Kariuki na taarifa kamili.

 (Ripoti ya Alice)

Ripoti hiyo iliyozinduliwa kwenye makao makuu ya FAO mjini Roma Italia kwa ushirikiano na makao makuu ya UNEP mjini Nairobi Kenya inaonyesha kuwa karibu tani bilioni mbili za chakula hutupwa kila mwaka hali ambayo haiathiri tu uchumi bali pia maliasili ambayo ni tegemeo kubwa kwa binadamu. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti  huko Roma, Mkurugenzi mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva amesema matumizi mabaya ya chakula ni chanzo kikuu ya kutupwa kwa chakula hali ambayo husababisha kuwepo uzalishaji wa juu wa chakula na athari mazingira na hali ya hewa.

 (SAUTI YA DA SILVA)

 “Theluthi moja  ya chakula kinachozalkishwa hutupwa au hutumika kwa njia mbaya.  Watumiaji wa kila siku hususan kwenye nchi zilizoendelea hutumia vibaya chakula kingi sawia na chakula chote kinachozalishwa kusini mwa jangwa la sahara. Athari zinazotokana na matumizi mabaya kama haya kwa usalama wa chakula na ustawi ni kubwa. Kama tunaweza kupunguza kutupwa kwa chakula itakuwa njia bora ya kuzuia kutumika vibaya kwa mali asili.”

 Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Achim Steriner amesema matumizi ya chakula majumbani na hotelini ni suala linalohitaji kuchunguzwa ili kupunguza utupaji wa chakula.

 (Sauti ya Achim)

Mpango wetu ni kuwafikia watu kwenye nchi zote na mabara yote na kwenye sekta zote ili kuwa sehemu ya kutatua suala hili la kutumika vibaya kwa  chakula jambo ambalo halihitajiki wala kukubalika katika karne  ya ishirini na moja. Sisi zote tuna uwezo wa kutatua suala hili kwa kuwa sehemu ya suluhisho,

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa chakula kinachozalishwa bila kutumiwa  hutumia kiwango kikubwa zaidi cha maji na huchangia karibu tani bilioni 3.3 za gesi inayochafua hewa  kwenye anga ya dunia.