Viongozi mashuhuri Darfur wakutana kujadili suluhu ya migogoro ya kikabila

11 Septemba 2013

Mizozo ya mara kwa mara ya kikabila huko Darfur nchini Sudan imesababisha viongozi mashuhuri kwenye jimbo hilo kukutana na kujadili jinsi ya kuipatia suluhisho la kudumu hususan kuwezesha makabila hayo kuishi kwa amani na utangamano.

Mkutano huo ulioandaliwa na ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika huko Darfur, UNAMID ulileta pamoja washiriki zaidi ya 100 wakiwemo wabunge, magavana, mawaziri na wawakilishi wa vikundi vya kiraia.

Naibu mkuu wa UNAMID Joseph Mutaboba akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano amesema viongozi hao wakiwa ni viongozi muhimu wa kisiasa, kijamii na kitaalamu huko Darfur wameonyesha utayari wao wa kushughuli mizozo hiyo ya kikabila ya mara kwa mara. Amesema amani ya kijamii na kuishi kwa utangamano ni misingi ya usalama, utulivu na maendeleo.

Miongoni mwa mapendekezo ya viongozi hao katika kupatia suluhu mzozo huo ni kupokonya watu silaha, na kutunga sheria ambazo zitaweka utangamano kati ya wakulima na wafugaji na kupatia suluhu mizozo ya ardhi.