Liberia inasonga mbele licha ya changamoto: Mkuu UNMIL

10 Septemba 2013

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limepatiwa ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu hali ilivyo nchini Liberia miaka kumi baada ya mlolongo wa makubaliano ya amani kutiwa saini huko Accra, Ghana. Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Liberia, UNMIL Karin Landgren amesema Liberia yapaswa kupongezwa na zaidi ya yote yahitaji usaidizi kwani muongo mmoja ni mkubwa zaidi kuhifadhi amani lakini ni kipindi kifupi sana kuondoa athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosambaratisha nchi hiyo.

Amesema vichocheo vingi vya mgogoro bado havijashughulikiwa ikiwemo masuala ya umiliki wa ardhi na matumizi ya maliasili kwa ajili ya uchumi wa nchi hiyo, lakini kubwa zaidi ni rushwa.

(Sauti ya Karin)

Kuhusu ulinzi amesema tayari walinda amani wa UNMIL wameondoka maeneo Kumi na Moja ambapo maeneo Nane kati ya hayo yako chini ya polisi wa Liberia lakini ukata unakwamisha operesheni zao.

(Sauti ya Karin)

Amesihi jumuiya ya kimataifa kuongeza usaidizi wake hususan wa kifedha kwa Liberia ili iweze kuimarisha taasisi zake za ulinzi na usalama na kusongesha mbele maendeleo ya nchi.