Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Itakuwa vyema Syria ikikabidhi silaha zake za kemikali: Ban

Itakuwa vyema Syria ikikabidhi silaha zake za kemikali: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema pendekezo la Urusi kwa Syria kuweka silaha zake za kemikali chini ya uangalizi wa kimataifa ni zuri na kwamba iwapo Syria itakubali, jumuiya ya kimataifa itachukua hatua haraka kutekeleza mpango huo.

Bwana Ban amesema hayo wakati akijibu swali la waandishi wa habari mjini New York, Marekani baada ya kuwapatia muhtasari wa ziara yake huko St. Petersburg, Urusi ambako alitumia fursa ya mkutano wa kundi la nchi 20 kupigia chepuo amani na usaidizi wa kibinadamu Syria. Katibu Mkuu amesema suala usimamizi na kuteketeza silaha za Syria ni moja ya mambo ambayo amekuwa akizingatia ili kupendekeza kwa Baraza la Usalama.

(Sauti ya Ban-1)

“Nina mpango wa kuliomba baraza la usalama kuitaka Syria ihamishe haraka silaha zake zote za kemikali na vifaa husika kwenda maeneo ndani ya Syria ambako zinaweza kuhifadhiwa kwa usalama na kuteketezwa. Naisihi tena Syria iwe mwanachama wa shirika la kimataifa la kupiga marufuku silaha za kemikali. OPCW.”

Na kuhusu matokeo ya uchunguzi Katibu Mkuu amesema bado hajapokea ripoti ya uchunguzi wa madai ya matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria unaofanywa na jopo linaloongozwa na Dkt. Ake Sellstrom, lakini tayari ana mapendekezo yake kwa Baraza la Usalama iwapo uchunguzi huo utabaini kuwa silaha zilitumika.

(Sauti ya Ban-2)

“Tayari ninafikiria mapendekezo yangu kwa baraza la usalama wakati nawasilisha matokeo ya uchunguzi. Kutakuwa na suala la uwajibikaji: kwa wale waliotumia iwapo uchunguzi utathibitisha yalitumika na halikadhalika kuzuia mtu yeyote asitumie tena njia hii ya kikatili. Na bado kuna umuhimu mkubwa wa kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa Geneva na kumaliza uhasama. Wananchi wa Syria wanahitaji amani.”

Assumpta Massoi