Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yaya Toure apeperusha bendera kuokoa Tembo wa Afrika

Yaya Toure apeperusha bendera kuokoa Tembo wa Afrika

Balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira, UNEP ambaye pia ni mwanasoka nyota ulimwenguni kutoka Cote d’Ivoire, Yaya Toure ametumia mechi ya kusaka kufuzu kucheza kombe la dunia kati ya timu yake ya Taifa na ile ya Morocco kutuma ujumbe thabiti dhidi ya ujangili wa tembo barani Afrika. George Njogopa na taarifa kamili

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Mchezo huo ambao ulinunuliwa rasmi na kufuatiliwa na watazamaji zaidi ya milioni 24 duniani kote, ulitoa fursa kwa wachezaji kutuma ujumbe wa kupambana na vitendo vya uwindaji haramu wa tembo. Wakiwa wamepandisha bendera juu wachezaji hao waliwasilisha kauli mbio inayohimiza uelewa wa kuwajali tembo na wanyama wengine wa mwituni ambao wanakabiliwa na kitisho cha kutoweka kutokana na kuongezeka wimbi la uwindaji haramu. Akizungumza wakati wa mchezo huo wa soka, mchezaji wa kimataifa Yaya Toure, alisema kuwa Afrika inakabiliwa na kitisho cha kupoteza tembo wote hatua ambayo inaweza kuathiri shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo maeneo ambayo yanawatumia wanyama hao kama sehemu yake ya utalii.Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya tembo 17,000 waliuwawa katika kipindi cha mwaka 2011 na kuna uwezekano idadi hiyo pengine ikawa kubwa ya hiyo.Ripoti zinaonyesha kuwa vitendo vya uwindaji haramu vimeshika kasi katika nchi za Afrika ya Kati. Idadi ya tembo inaripotiwa kupungua katika mataifa mengi ya afrika, na huko nchini Cote d’Ivoire tembo walioko sasa wanafikia 800. Katika eneo la Kaskazini mwa Cameroon kiasi cha tembo waliouliwa na makundi ya waasi kutoka nchi za Chad na Sudan walifikia 450.