Mwendesha mashtaka kesi dhidi ya Ruto akubaliwa kukata rufaa

6 Septemba 2013

Jopo la majaji katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague, Uholanzi limeridhia ombi la mwendesha mashtaka katika kesi dhidi ya William Ruto na Joshua Arap Sang la kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa jopo hilo wa kukataa abadili hati ya mashtaka ya muda dhidi ya watuhumiwa hao.

Awali mashtaka dhidi yao yalithibitishwa tarehe 23 mwezi Januari mwaka huu na jopo hilo na kutangazwa kuwa kesi yao itaanza kusikilizwa. Hata hivyo mwendesha mashtaka tarehe 22 Julai aliomba kibali kubadili hati ya mashtaka dhidi ya wawili hao kwa kupanua wigo wa makosa kuhusiana na uhalifu wanaodaiwa kutenda kwenye eneo la Eldoret tarehe 30 na 31 mwezi Disemba mwaka 2007.

Jopo la majaji awali lilikataa ombi hilo kwa maelezo kuwa mwendesha mashtaka alichelewesha ombi lake, athari za hatua hiyo kwa upande wa utetezi, haki na uharaka wa mchakato mzima wa kesi hiyo.

Uamuzi wa leo sasa unaupatia upande wa mashtaka kukata rufaa iwapo jopo la majaji lilitumia vibaya mamlaka yake ya kuweza kukubali au kukataa ombi hilo. Kesi dhidi ya Ruto na Sang imepangwa kuanza kusikilizwa tarehe 10 mwezi huu.