Hali ya kibinadamu Syria ni mbaya, misaada zaidi yahitajika: Ban

6 Septemba 2013

Huko St. Petersburg nchini Urusi, ambako kando mwa mkutano wa viongozi wa kundi la G20, hii leo kumefanyika mkutano wa kujadili misaada ya kibinadamu kwa Syria, ulioandaliwa na Uingereza. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameshiriki mkutano huo ambapo ametaka nchi hizo 20 kushawishi pande husika kwenye mzozo wa Syria kuruhusu watoa misaada kuwafikia wahitaji na kubwa Zaidi mzozo huo umalizwe kisiasa na si kijeshi. Ripoti ya Alice Kariuki inafafanua Zaidi.

 (RIPOTI YA ALICE KARIUKI)

Miaka miwili iliyopita hakuna aliyedhani Syria ingefika hapa, ni Katibu Mkuu Ban Ki-moon kwenye hotuba yake kwa washiriki wa mkutano huo ambapo amesema hivi sasa hali ya usalama, kibinadamu ni mbaya mamilioni kadhaa ya Wasyria ni wakimbizi wa ndani na wengine wako nchi jirani.

Amesema mahitaji yanaongezeka kila uchwao lakini jitihada za Umoja wa Mataifa kufikisha hata kile kidogo ilichonacho kwa wahusika ni ngumu kutokana na hali ya usalama kuzorota. Bwana Ban amesema ushawishi wa nchi hizo kwa pande zote Syria ni muhimu sambamba na uchangiaji wa fedha za misaada ya kibinadamu.

 (CLIP YA BAN KI-MOON)

 "Hivyo basi nawasihi mshirikiane na wahisani wanaoibukia kuongeza msaada wa Umoja wa Mataifa na kubuni njia mpya za kusaidia kwa kuwa bajeti ya sasa ya msaada hailingani na mahitaji mapya yanayoongezeka. Wakati baadhi wanakimbia nchi yao, wengine wanazidi kupigana. Lazima nionye kuwa fikra potofu ya nguvu za kijeshi itasababisha madhara makubwa na ongezeko la tishio la ghasia za kidini. Suluhu thabiti ya kisiasa Syria ni lazima itokane na utekelezaji kamili wa makubaliano ya Geneva”