Uongozi wa G-20 ni muhimu katika kuimarisha uchumi duniani: Ban

5 Septemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema kundi la nchi 20 au G20 lina nafasi muhimu katika kuimarisha mipango ya kujikwamua kiuchumi duniani wakati huu ambapo mizozo katika eneo moja inakuwa na athari hata kwa nchi tajiri zaidi duniani. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kauli hiyo ya Bwana Ban imo katika barua aliyowaandikia viongozi wa mataifa 20 wanaokutana huko St. Petersburg nchini Urusi kwa siku mbili kuanzia leo. Barua hiyo ya Bwana Ban imegusia uharakishaji wa malengo ya maendeleo ya milenia, ukosefu wa ajira, mabadiliko ya tabia nchi na ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015 itakapofikia ukomo wa malengo ya milenia. Bwana Ban amesema viongozi wa G20 wana nafasi kubwa kuimarisha mikakati ya kujikwamua na changamoto zinazofanya kasi ya maendeleo kusuasua. Amesema sasa ni wakati wa kutokomeza umaskini katika dunia ya leo iliyounganika ambapo mizozo ya karibuni imeathiri nchi tajiri na kugharimu maisha ya kijamii na makundi yaliyo hatarini. Bwana Ban ametaka sera thabiti za kukuza uchumi na kutoa fursa za ajira.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter