Nchi zinazohifadhi wakimbizi na UNHCR kujadili mgogoro wa Syria

4 Septemba 2013

Mawaziri wa nchi kutoka Iraq, Jordan, Lebanon na Uturuki  wanakutana mjini Geneva leo Jumatano kushiriki mkutano kuhusu matatizo ya wakimbizi wa Syria, mkutano unaongozwa na kamishina mkuu wa wakimbizi António Guterres.

Mkutano huo unafanyika siku moja baada ya idadi ya Wasyria walioorodheshwa kama wakimbizi au wanaosubiri kuorodheshwa imepindukia milioni 2, na Shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR linasema linatiwa hofu na kuendelea kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika nchi hiyo, na athari zake kwa nchi zinazohifadhi wakimbizi wengi wa Syria.

Lebanon,Jordan,Turkey na Iraq ni nchi nne zinazohifadhi wakimbizi wengi wa Syria. Zaidi ya asilimia 97 ya wakimbizi wa Syria wanahifadhiwa katika nchi jirani na hivyo kuzibebesha mzigo mkubwa katika miundombinu, uchumi na jamii kwa ujumla, na hivyo zinahitaji msaada mkubwa wa kimataifa.

Kamisha mkuu na viongozi wa nchi hizo nne mkutano wao unafungua njia ya mkutano wa mawaziri unaotarajiwa kufanyika Septemba 30 kama sehemu ya mkutano wa kamati ya UNHCR wa kila mwaka. Lengo litakuwa ni kuafikiana suluhu ya muda mrefu na msaada wa dharura wakihusisha pia taassisi za fedha za kimataifa.