Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu ya usalama wa Taifa kamwe isiwe halalisho la kutisha waandishi wa habari

Hofu ya usalama wa Taifa kamwe isiwe halalisho la kutisha waandishi wa habari

Wataalamu wawili huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kujieleza na udhibiti wa ugaidi wametaka maelezo zaidi kutoka serikali ya Uingereza kufuatia tukio la hivi karibuni la mwandishi wa habari David Miranda, mshirika mwa mwandishi Glenn Greewald wa gazeti la Guardian kushikiliwa kwa saa kadha kwenye uwanja wa ndege wa Heathrow na vifaa vyake vya kazi kuchukuliwa na vingine kuharibiwa.

Wataalamu Frank la Rue wa uhuru wa kujieleza na Ben Emmerson wa vita dhidi ya ugaidi wamesema ni wazi kuwa utunzaji wa siri za taifa kamwe usiwe kisingizio cha kukandamiza uhuru wa vyombo vya h abari

Wamesema vyombo vya habari vina dhima kuu katika kuelezea ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba iko wazi hivi sasa kuwa hatua za baadhi ya serikali za kufuatilia usalama wa Taifa zinapaswa kujadiliwa.

Wamesema tathmini ya sasa ya vitisho vya ugaidi kwa Uingereza imebadilika kwa miaka mitatu iliyopita na hivyo kuna umuhimu wa kuanzisha mjadala wa wazi kuona ni kwa kiasi gani umma unaweza kuvumilia kitendo cha mamlaka za dola kuingilia taarifa zao. Bwana Emmerson ametaka serikali ya Uingereza kuangalia upya sheria zake ili zikidhi viwango vya Umoja wa Ulaya kuhusu haki ya uhuru, usalama na kuingilia faragha ya mtu.