Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio lolote dhidi ya Syria bila idhini ya Baraza la Usalama ni batili: Ban

Shambulio lolote dhidi ya Syria bila idhini ya Baraza la Usalama ni batili: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amekutana na waandishi wa habari mjini New York, Marekani hii leo ambapo suala kuu lilikuwa ni kutoa taarifa kuhusu hatua zilizofikiwa za uchunguzi wa silaha za kemikali zinazodaiwa kutumika kwenye eneo la Ghouta, nchiniSyriawiki mbili zilizopita. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.

 (Taarifa ya Assumpta)

 Mkutano huo ulisubiriwa kwa hamu na waandishi wa habari kwa kuzingatia kuwa hii leo Bwana Ban amekutana na wajumbe 10 wasio wa kudumu ndani ya baraza la usalama na wiki iliyopita alikutana na wale watano wa kudumu ambao ni Urusi, China, Marekani, Ufaransa na Uingereza. Katika mkutano huo na waandishi wa habari Bwana Ban akasema kuwa jopo linaloongozwa na Profesa Ake Sellestrom linaendelea na kazi yake kutwa huko Uholanzi.

 (Sauti ya Ban)

 “Jopo linafanya kazi kutwa kucha tangu lirejee kutoka Syria likiandaa sampuli ilizokusanya kwa ajili ya uchunguzi. Ninapenda kutangaza kuwa sampuli zote za kibaolojia na kimazingira zitakuwa zimewasilishwa kwenye maabara husika kesho.”

 Bwana Ban amesema kuwa uchunguzi huo utakapokamilia atatoa taarifa mara moja kwa wanachama wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama na akasisitiza…

 (Sauti ya Ban)

 “Kama nilivyosisitiza kila wakati, iwapo matumizi yoyote ya silaha za kemikali yatathibishwa, itakuwa ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa na uhalifu mkubwa wa kivita. Karibu muongo mmoja uliopita baada ya machungu ya vita vya kwanza jumuiya ya kimataifa ilipiga marufuku matumizi ya silaha hizi za maangamizi. Ubinadamu wetu unatushinikiza kuhakikisha silaha za kemikali hazitumiki vitani au kwa ugaidi kwenye karne hii ya 21. Wahusika wowote  hawapaswi kukwepa sheria.”

 Halikadhalika Katibu Mkuu akarejelea wito wake kuwa shambulizi lolote dhidi yaSyriabila idhini ya baraza la usalama ni batili na akatoa wito kwa wajumbe wa barazahilo..

 (Sauti ya Ban)

 “Nawasihi wanachama wote kuungana na kuchukua hatua sahihi iwapo matumizi ya silaha za kemikali yatathibitishwa.”

 Katibu Mkuu ameondoka mchana huu kwenda St. Petersburg, Urusi kushiriki mkutano wa kundi la nchi 20 ambapo amesema atatumia mkutano huo kujadili mustakhbali wa misaada ya kibinadamu huko Syria.