Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sintofahamu nchini Syria, Ban anashauriana na wajumbe wa kudumu wa Baraza la usalama

Sintofahamu nchini Syria, Ban anashauriana na wajumbe wa kudumu wa Baraza la usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ambaye amekatiza ziara yake huko Austria na kurejea New York, Marekani kwa ajili  ya kushughulikia suala la Syria hivi sasa yuko katika mashauriano na nchi tano zenye ujumbe wa kudumu katika baraza la usalama la umoja huo. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nersiky amewaambia waandishi wa habari kuwa amewapatia muhtasari wa kazi inayofanywa na jopo la uchunguzi wa silaha za kemikali huko Syria linaloongozwa na Profesa Ake Sellstrom hususan kwenye eneo la Ghouta, lililokumbwa na shambulio  tarehe 21 mwezi huu. Bwana Nersiky amesema hii leo jopohilolimetembelea hospitali ya kijeshi inayomilikiwa na serikali huko Damascus.

 (Sauti ya Martin)

 “Katibu Mkuu pia amekuwa akiwaelezea  wajumbe hao wa kudumu kuwa katika ukaguzi huo jopo liliweza kutembelea hospitali na kuhoji wagonjwa, madaktari na hata na maeneo yaliyoathiriwa na kuhoji mashuhuda na  kukusanya sampuli za ushahidi kutoka katika mazingira.”

 Msemaji huyo amesema ukusanyaji wa sampuli na ushahidi vimeshakusanywa na jopohilolitaondokaSyriakesho kuelekea The Hague ambako ni makao makuu ya shirika la kimataifa la kupinga matumizi ya silaha za kemikali.

 (Sauti ya Martin)

 “Sampuli zilizokusanywa zitapelekwa kufanyiwa uchunguzi katika maabara maalum za uchunguzi kwa lengo la kuharakisha uchunguzi wa sampuli zilizochukuliwa. Lakini ni vyema tuelewe vyema kabla jopo hilo halijatoa hitimisho lolote kuhusu tukio hilo, uchunguzi wa sampuli katika maabara zote ni lazima uwe umekamilika.”

 Mwakilishi wa Katibu Mkuu kuhusu kuzuia kuenea kwa silaha, Angela Kane ambaye naye alikuwaSyriaameshaondoka na kesho Jumamosi atakutana na Bwana Ban kumjulisha shughuli ilivyokwenda.