Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakaguzi wa UM kukabidhi ripoti ya uchunguzi Syria Jumamosi: Ban

Wakaguzi wa UM kukabidhi ripoti ya uchunguzi Syria Jumamosi: Ban

Jopo la Umoja wa Mataifa linalochunguza madai ya shambulizi la silaha za kemikali nchini Syria litakabidhi ripoti hiyo Jumamosi hii kwa Katibu Mkuu Ban Ki-Moon. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu Ban Ki-Moon mwenyewe alizotoa alipozungumza na waandishi wa habari mjini Vienna, Austria ambako yuko ziarani. Bwana Ban amesema suala hilo la Syria amekuwa akifanya mashauriano na viongozi mbali mbali duniani akiwemo Rais Barack Obama wa Marekani, ambaye Jumatano wamezungumza juu ya amani na majadiliano nchini Syria. Halikadhalika wamejadili jinsi ya Umoja wa Mataifa na nchi zingie hususan Marekani zinaweza kushirikiana kuharakisha uchunguzi wa silaha za kemikali Syria. Bwana Ban akaulizwa kuhusu suala la shambulio la kijeshi kabla ya ripoti ya uchunguzi….

(Sauti ya Ban)

“Ni muhimu tofauti zote za maoni zikapatiwa suluhu kwa njia ya amani na kwa mashauriano na nitaendelea kufanyia kazi msingi huu. Wakaguzi wataendelea na kazi yao hadi kesho Ijumaa na wataondoka Syria Jumamosi asubuhi na kunipatia ripoti punde tu wakitoka Syria. Nddio maana nimekatiza ziara yangu Austria.”

Katibu Mkuu amesema amemhakikishia Rais Obama kuwa taarifa za uchunguzi na ushahidi wowote ule kuhusu kemikali kutoka Syria zitapatiwa wajumbe wa Baraza la Usalama na nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa.