Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kasri ya amani The Hague yatimiza miaka 100, Ban azungumzia utawala wa sheria

Kasri ya amani The Hague yatimiza miaka 100, Ban azungumzia utawala wa sheria

Leo ni maadhimisho ya miaka mia moja tangu ujenzi wa kasri la amani lililoko The Hague Uholanzi, lenye ofisi za masuala ya sheria ikiwemo mahakama ya haki ya Umoja wa Mataifa. Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon aliyeelekeza hotuba yake zaidi kwenye masuala ya amani, usalama duniani na umuhimu wa utawala wa sheria. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Tunaondoka katika zama za ukwepaji mkono wa sheria na kuelekea zama mpya za kuwajibika na matendo tunayofanya, ni kauli ya Bwana Ban kwenye sherehe hizo huko The Hague , mji ambao kutokana kuwa makazi ya vyombo vya kisheria vya Umoja wa Mataifa ikiwemo mahakama ya kimataifa ya haki umetambuliwa kama kitovu cha haki na mji mkuu wa dunia kwa masuala ya sheria. Bwana Ban akazungumzia mwelekeo wa haki duniani hivi sasa kwa kuzingatia uwepo wa vyombo hivyoThe Hague.

 (Sauti ya Ban)

“Ushahidi umeonyesha utashi wa dunia hivi sasa wa kuwawajibisha wakosaji bila kujali nyadhifa au umaarufu wao. Na uwepo wa mahakama hizi umeanza kuzuia vitendo vya uhalifu vya baadaye. Hofu ya kuishia The Hague imekuwa dhahiri. Wanalazimika kufirikia kwa dhati kabla ya kufanya kosa lolote. Lakini ni muhimu kwa nchi kuendeleza kasi hii hasa kwa kusaini mkataba wa kuanzisha ICC na kuonyesha ushirikiano na mamlaka za kisheria za kimataifa.”