Feltman na viongozi wa Iran wajadili suala la Syria

27 Agosti 2013

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya siasa, Jeffrey Feltman amehitimisha ziara yake nchini Iran ambapo miongoni mwa mambo yaliyojitokeza wakati wa mazungumzo yake na viongozi waandamizi wa nchi hiyo ni hatma ya mgogoro wa Syria na nafasi ya Iran katika kupatia suluhu mzozo huo unaozidi kuathiri eneo la Mashariki ya Kati.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amemkariri Bwana Feltman akisisitiza msimamo wa Umoja huo wa kupinga matumizi ya nguvu za kijeshi katika kutatua mzozo huo na badala yake kuelezea matumaini ya kufanyika kwa mkutano wa pili wa Geneva kuhusu amani nchini Syria. Halikadhalika alielezea matarajio ya Umoja wa Mataifa kwa Iran.

(Sauti ya Farhan)

“Bwana Feltman alielezea msimamo wa Umoja wa Mataifa ya kwamba Iran kwa kuzingatia ushawishi wake na uongozi kwenye eneo hilo ina dhima kubwa ya kusaidia kuleta pande zinazopingana nchini Syria kwenye meza ya mazungumzo kwa kuzingatia mpango wa Geneva. Pia alishukuru taarifa za viongozi wa Iran za kutumia njia za amani kumaliza mzozo wa Syria.”