Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi wa kemikali za silaha Syria waahirishwa kwa siku moja

Uchunguzi wa kemikali za silaha Syria waahirishwa kwa siku moja

Kazi ya kuchunguza madai ya uwepo wa silaha za kemikali kwenye eneo moja karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus, imeahirishwa kwa leo Jumanne baada ya uchunguzi kufanyika hapo jana. Assumpta Massoi na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Umoja wa Mataifa umesema jopo hilo likiongozwa na Profesa Ake Sellstrom lilikuwa liendelee na kazi hiyo Jumanne lakini shambulio la Jumatatu la kuvizia dhidi ya msafara wao limefanya kazi iahirishwe ili kutoa fursa za maandalizi ya kuimarisha usalama.

Katika taarifa kwa waandishi wa habari, Umoja wa Mataifa umesema kwa kuzingatia mazingira tata kwenye eneo hilo, kibali cha kwenda bado hakijatolewa penginepo baadaye leo.

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon ameendelea kusisitiza pande zote kwenye mzozo nchini Syria kuhakikisha jopo la uchunguzi linafanya kazi yake kwa usalama na uhakika.