Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakaguzi wa UM watembelea hospitali huko Damascus

Wakaguzi wa UM watembelea hospitali huko Damascus

Hatimaye jopo la wakaguzi wa Umoja wa Mataifa limeweza kuendelea na kazi yake kwenye eneo linalodaiwa kuwa na silaha za kemikali kwenye viunga vya mji mkuu wa Syria, Damascus baada ya kushambuliwa na mshambuliaji wa kuvizia leo asubuhi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari mjini New York, hii leo kuwa gari lililokuwa mbele lilitunguliwa na kuharibika na hivyo kulazimika kwenda kubadilisha na hatimaye jopo hilo linaloongozwa na Profesa Ake Sellstrom liliendelea na kazi yake.

(Sauti ya Farhan)

Jopo hilo limerejea kwenye eneo hilo na limetembelea baadhi ya hospitali kwenye eneo hilo. Na inapaswa kusisitizwa tena kuwa pande zote zinapaswa kutoa ushirikiano ili jopo hilo liweze kufanya kazi yake muhimmu kwa usalama.”

Tayari Katibu Mkuu Ban Ki-moon amezungumza na mwakilishi wake kuhusu kuzuia kuenea kwa silaha, Angela Kane ili awasilishe malalamiko rasmi kwa serikali ya Syria na mamlaka za vikundi vya upinzani ili hali hiyo isitokee tena.