Maoni ya umma dhidi ya haki za binadamu DRPK yanasisimua: Kirby

26 Agosti 2013

Jopo la Umoja wa Mataifa lililoundwa kuchunguza hali ya haki za binadamu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korera, DRPK kesho jumanne linaondoka Seoul Korea kusini kuelekea Tokyo baada ya kuhitimisha kazi ya kupokea maoni ya umma. Taarifa ya Grace Kaneiya inafafanua zaidi.

(RIPOTI YA GRACE KANEIYA)

Jopo hilo likiongozwa na Michael Kirby lipo nchini Korea Kusini kwa siku kumi ambapo hadi sasa zaidi ya mashuhuda 40 wameelezea kile walichokiona huko Korea Kaskazini au DPRK.

Bwana Kirby anasema kwa kipindi chote hicho mashuhuda wametoa shuhuda makini na za kina zilizostaajabisha jopo hilo la watu watatu. Kwa mantiki hiyo wametoa shukrani kwa wote waliokuwa jasiri na kujitokeza kutoa shuhuda kuhusu machungu waliyopitia wakiwa DPRK.

Kutoka Seoul, jopo hilo litaelekea Tokyo, Japan kwa shughuli hiyo hiyo ya kukusanya maoni ya umma. Mambo yanayochunguzwa ni pamoja na kutekwa nyara kwa raia wa Japan kwenda DPRK.