Kuzorota kwa hali ya usalama Jonglei kwatia wasiwasi Baraza la Usalama

Kuzorota kwa hali ya usalama Jonglei kwatia wasiwasi Baraza la Usalama

Kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama kwenye jimbo la Jonglei, Sudan Kusini kumeibua wasiwasi miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo hii leo wametaka pande zote zinazopingana eneo hilo kuheshimu haki za binadamu. Taarifa iliyosomwa na Rais wa baraza hilo Balozi María Cristina Perceval baada ya mashaurino baina yao, imekariri wajumbe wakisema hali ya usalama na ya kibinadamu inazorota kila uchwao , mashambulizi dhidi ya raia na uporaji wa mali katika ofisi za Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada vinatia wasiwasi. Wajumbe wamesema mashambulizi yanazidi kufanya raia kukimbia makaziyaona hata jitihada za kuwafikia kutoa misaada zinakumbana na vikwazo. Hivyo wakatoa ombi.

 (Sauti ya Balozi)

 “Wameshutumu suala kwamba mashambulio hayo yanasababisha wakimbizi wa ndani miongoni mwa raia na kuitaka serikali ya Sudan Kusini ambayo ina wajibu wa kulinda raia, kuharakisha uwezekano wa kuwasilisha misaada ya kwa usalama na bila vikwazo vyovyote na kwa raia wote wanaohitaji misaada ya dharura kwa mujibu wa vipengele vya sheria ya kimataifa.”

Kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali ya Sudan Kusini dhidi ya baadhi ya watendaji wa jeshi la nchi hiyo wanakiuka maadili, Balozi Perceval anasema….

(Sauti ya Balozi)

“Wametambua azma ya Rais Kiir ya kuchunguza na kuwajibisha wale wanaotuhumiwa kukiuka haki za raia huko Jonglei na wamerejelea hofu  yao kubwa juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na vikundi vyenye silaha na taasisi za usalama za taifa ikiwemo baadhi ya watendaji wa SPLA.”