Ban alaani mashambulizi ya mabomu nchini Lebanon:

23 Agosti 2013

KM Ban Ki-moonKatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali milipuko miwili ya mabomu yaliyokuwa yametegwa kwenye magari nje ya misikiti miwili mjini Tripoli Kasakazini mwa Lebanon.

Milipuko hiyo imekatili maisha ya makumi ya watu na kujeruhi wengine kwa mamia muda mfupi baada ya swala ya Ijumaa. Ban ametuma salamu za rambiorambi kwa familia za waliopoteza maisha , kwa serikali ya Lebanon na kuwapa pole wote waliojeruhiwa.

Ameitaka serikali ya Lebanon kujizuia na kusalia katika mshikamano, na kusaidia taasisi zake ,husuani majeshi ya ulinzi na usalama ili waweze kuhakikisha utulivu Tripoli na nchi nzima.

Pia ameitaka serikali kuhakikisha inazuia kutokea tena kwa matukio kama hayo na anatumai kwamba wale waliohusika na ukatili huo watafikishwa kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo. Ameongeza kuwa jumuiya ya kimataifa imejizatiti kuisaidia Lebanon kuimarisha usalama na utulivu.