Olimpiki 2016 Rio kujali mazingira na uendelevu: UNEP

20 Agosti 2013

Suala la uhifadhi wa mazingira na kuwa na dunia endelevu wakati wa michezo ya olimpiki ya mwaka 2016 itakayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazili limepatiwa chepuo baada ya kamati ya maandalizi ya michezo hiyo na shirika la mazingira la

Umoja wa Mataifa kukubaliana mikakati mipya juu ya suala hilo.

Chini ya makubaliano hayo UNEP itasaidia mchakato kwa kutoa wataalamu wa kiufundi kuhusu uhifadhi wa mazingira wakati wa maandalizi na kipindi chote cha michezo kwa ubia pia na serikali ya Brazil. Tayari nembo inayotilia mkazo suala la dunia endelevu imeshazinduliwa na kamati ya maandalizi na itatumika kwenye vifaa husika na vikasha vya taarifa kwa ajili ya kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Rais wa kamati ya maandalizi ya Rio 2016 Carlos Arthur Nuzman amesma michezo inapaswa kuwa mstari wa mbele kuendeleza dunia endelevu huku Denise Hamu mwakilishi wa UNEP, Brazil akisema kuwa michezo na mazingira ni vitu muhimu kwa maendeleo endelevu. Mwaka 1999 kamati ya kimataifa ya olimpiki ilianzisha ajenda yake ya kujumuisha misingi ya uendelevu katika operesheni zake.