Mkataba wa kimataifa kuhusu ajira za majini waanza kutumika rasmi leo: ILO/

20 Agosti 2013

Mkataba wa kimataifa kuhusu ajira za wafanyakazi kwenye vyombo vya majini uliokuwa ukipigiwa chepuo na shirika la kazi duniani, ILO umeanza kutumika rasmi leo tarehe 20 Agosti 2013.

Mkurugenzi Nkuu wa ILO Guy Rider amesema hizo ni habari njema na kwamba mkataba huo ni wa kihistoria kwani unalenga pamoja na mambo mengine kuhakikisha mazingira bora ya kazi na utu kwa mabaharia na wakati huo huo unaweka uwiano wa biashara kwa wamiliki wa meli kwenye sekta ya usafirishaji majini duniani.

Bwana Ryder ametaka nchi zote zenye maslahi ya usafirishaji kwa njia ya maji kuridhia mkataba huo iwapo hazijafanya hivyo huku akisihi serikali na wamiliki wa meli kufanya kazi kwa pamoja kutekeleza mkataba huo.

Mkataba huo ulihitishaji kuridhiwa na mataifa 30 wanachama wa ILO lakini tayari nchi 45 zimesharidhia. Ilichukua miaka mitano ya maandalizi hadi kupitishwa kwa mkataba huo ambao unaungwa mkono na shirikisho la vyama vya mabaharia duniani, ITF na lile la wamiliki wameli, ISF.