Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko uchaguzi Mali, kilichobakia kuimarisha taasisi na utulivu: Wajumbe Baraza la usalama

Heko uchaguzi Mali, kilichobakia kuimarisha taasisi na utulivu: Wajumbe Baraza la usalama

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wamezingatia matokeo ya awamu ya pili ya uchaguzi nchini Mali kama yalivyotangazwa na mamlaka za mpito nchini humo ambapo Ibrahim Boubacar Keïta ametangazwa mshindi wa Urais wa nchi hiyo. Kwa mantiki hiyo wajumbe hao wamesifu wananchi wa Mali kwa jinsi walivyoshiriki kwenye mchakato wa uchaguzi kwa amani. Halikadhalika wametoa heko kwa mamlaka za mpito pamoja na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA kwa usaidizi wake wote wakati wa mchakato huo bila kusahau wabia wa kitaifa na kimataifa. Akisoma taarifa kwa niaba ya wajumbe hao, Rais wa Baraza la Usalama Balozi Maria Cristina Perceval wa Argentina amesema wajumbe wanataka pia kufanyika kwa uchaguzi huru, haki na jumuishi wa wabunge na kwamba ili kufanikisha hilo jambo muhimu ni kuimarisha amani na utulivu nchini Mali.

(Sauti ya Balozi Perceval)

Wanachama wa Baraza la Usalama wanasisitiza azimio namba 2100 la mwaka 2013 na kwa mantiki hiyo wanasisitiza umuhimu wa vikosi vya MINUSMA kusambazwa kwenye maeneo muhimu ya raia hususan kaskazini mwa Mali na kusaidia uanzishaji upya wa taasisi za umma nchini kote na kuendelea kutekeleza mpango wa kuleta amani, utawala wa sheria na usimamizi wa haki za binadaamu.”