Baraza la Usalama lataka machafuko yakomeshwe Misri

16 Agosti 2013

Wanachama wa Baraza la Usalama wameelezea kusikitishwa na watu kufariki nchini Misri na kutaka machafuko yakomeshwe. Kwa mujibu wa taarifa ilosomwa na rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Agosti, Bi María Cristina Percevalwa Argentina, wanachama wa Baraza hilo wameelezea maombolezo yao kwa wahanga wa machafuko hayo.

Kabla ya kufanya mazungumzo hayo ya faragha, Baraza hilo la Usalama limehutubiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson.

Bi Perceval amesema, mtazamo wa wanachama wa Baraza la Usalama ni kwamba pande zote nchini Misri zijizuie kwa vyovyote vile, na kukomesha machafuko na kuendeleza maridhiano ya kitaifa.

Akizungumza kwa niaba ya serikali ya Argentina, rais huyo wa Baraza la Usalama amelaani kupinduliwa kwa serikali nchini Misri, na kulaani ukandamizaji wa maandamano ya umma ambayo yamekuwa yakiendelea katika mitaa ya miji mikuu ya Misri, na ambayo yamekomeshwa kwa mauaji ya watu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter