Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wazindua Mkakati wa kusaidia maendeleo Ramallah

Umoja wa Mataifa wazindua Mkakati wa kusaidia maendeleo Ramallah

Umoja wa Mataifa umezindua mkakati wa kusaidia maendeleo, UNDAF, kama sehemu ya kuleta pamoja juhudi za mashirika yote ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Palestina, wakiwemo wakimbizi.

Akiuzindua mkakati huo mjini Ramallah, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema uzinduzi huo unaweka ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya watu na serikali ya Palestina na Umoja wa Mataifa.

“Hadi sasa, mashirika kumi na tisa ya Umoja wa Mataifa yanafanya kazi hapa. Kupitia kwa UNDAF, Umoja wa Mataifa unaunganisha juhudi zetu ili kutoa huduma bora zaidi kwa Wapalestina wote, wakiwemo wakimbizi. Nimefurahishwa na ajenda ya Palestina ya ujenzi wa taifa, ambayo UNDAF itaendelea kuunga mkono.”

Bwana Ban amesema watu wa Palestina wameonyesha dhahiri kuwa wana ari ya kutimiza ndoto zao, hata katika mazingira magumu, akitaja changamoto za Ukingo wa Magharibi kuendelea kukaliwa, ikiwemo Jerusalem Mashariki na Ukanda wa Gaza.

Amesema ni haki ya watu wa Palestina kutimiza lengo lao la kuishi katika taifa huru, na kwamba hilo ni muhimu kwa utulivu wa ukanda mzima, kwani pia ni lengo la Umoja wa Mataifa.