Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akutana na viongozi wa Palestina huko Ramallah, alaani shambulio Lebanon

Ban akutana na viongozi wa Palestina huko Ramallah, alaani shambulio Lebanon

Kuanza kwa mashauriano ya moja kwa moja kati ya Palestina na Israeli ni miongoni mwa ajenda za mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas mjini Ramallah. Bwana Ban amesifu uongozi wa Rais Abbas na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa kuwezesha kuanza tena kwa mazungumzo hayo ambapo amesema hiyo ndiyo njia pekee ya kufanikisha suala la mataifa mawili kwenye eneo hilo. Amesema ni matumaini yake kuwa mazungumzo hayo yatawezesha suluhu ya amani ya suala hilo.

Halikadhalika wamejadili hali ya hofu kwenye eneo linalokaliwa la Palestina ikiwemo suala al makazi na umuhimu wa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono zaidi mamlaka ya Palestina. Viongozi wengine aliokutana nao Bwana Ban ni Waziri Mkuu wa Palestina Rami Hamdalah na Waziri wa masuala ya magereza Isaa Qarage ambapo walijadili hali ya wafungwa wa Gaza kwenye magereza ya Israeli ikiwemo ugumu wanaopata jamaa zao wanapotaka kuwatembelea.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu amelaani shambulio lililofanyika kwenye viunga vya mji mkuu wa Lebanon, Beirut, na kusababisha vifo na majeruhi. Pamoja na kutuma rambirambi kwa wafiwa na pole kwa manusura, amesema mashambulio ya aina hiyo hayakubaliki akitumai kuwa wahusika watafikishwa mbele ya sheria.