Baraza la Usalama latiwa wasiwasi na hali ya usalama CAR

14 Agosti 2013

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali ya usalama katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako utaratibu wa kisheria umesambaratika katika mazingira ya ukosefu wa uongozi wa kisheria.

Mapema Jumatano asubuhi, Baraza hilo la Usalama limehutubiwa kuhusu hali nchini humo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kati, Babacar Gaye, Mratibu Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu, Valerie Amos na Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu Haki za Binadamu, Ivan Simonovic.

Katika taarifa ambayo imetolewa jioni baada ya kikao chao cha mchana, wanachama hao wa Baraza la Usalama wamesisitiza kuwa vita vya silaha na mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ni tishio kuu kwa utulivu nchini humo na kwa ukanda mzima.

Wameelezea pia wasiwasi wao kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu, pamoja na ukiukwaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na ripoti za kuenea kwa ukiukwaji wa haki za binadamu, hususan ule unaotekelezwa na makundi yanayohusiana na kundi la Séléka, kama vile kuwakamata na kuwazuilia watu kiholela, ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na watoto, utesaji, ubakaji, mauaji kinyume na sheria, utumiaji wa watoto vitani na mashambulizi dhidi ya raia.

Wamelaani vikali pia mashambulizi yanayowalenga wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.