Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano ya kikabila huko Darfur Mashariki yanaathiri zaidi raia: Mkuu UNAMID

Mapigano ya kikabila huko Darfur Mashariki yanaathiri zaidi raia: Mkuu UNAMID

Mwakilishi maalum wa ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika huko Darfur, UNAMID, Mohamed Ibn Chambas ameeleza wasiwasi wake vile ambavyo mapigano kati ya makabila ya Rezeiga na Ma’alia huko El Daein na Adila Darfur Mashariki yanavyozidi kuathiri raia.

Amesema mapigano hayo yanapaswa kusitishwa mara moja kwa maslahi ya pande zote kwani mapigano siyo suluhu na kwamba pande husika zimalize tofauti zao kwa njia za mazungumzo.

Bwana Chambas alikuwa akizungumza baada ya mkutano wake na Mwenyekiti wa mamlaka ya Darfur Dokta Eltijani Seisi. Mvutano kati ya makabila hayo mawili uliripotiwa kuibuka mapema mwezi huu juu ya mzozo wa ardhi na kwamba hali ya usalama inazidi kuzorota kwani mapigano yanasababisha vitendo vya uhalifu vinavyoathiri raia.

UNAMID imesaidia kuimarisha ulinzi huku ikiunga mkono jitihada zinazoendelea za mashauriano zinazoongozwa na serikali ili kuleta utulivu.