Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Familia nyingi za wakimbizi nchini Tanzania zinakabiliwa na tatizo la kudumaa-WFP

Familia nyingi za wakimbizi nchini Tanzania zinakabiliwa na tatizo la kudumaa-WFP

Zaidi ya asilimia 35 ya familia za wakimbizi walioko katika kambi ya Nyarugusu Mkoani Kigoma wanakabiliwa na tatizo la kudumaa kunakosababishwa na ukosefu wa lishe bora, jambo ambalo linatishia usalama wa afya za wakimbizi wengi.

George Njogopa na taarifa zaidi

Pamoja na tatizo hilo, pia baadhi ya wakimbizi wanadaiwa kuishi katika hali ngumu na wakati mwingine kuwa na wasiwasi wa kukosa misaada ya chakula kutokana na wafadhili wengi kusitisha baadhi ya huduma.

Akizungumzia hali ya wakimbizi katika mahojiano maalumu, Afisa Miradi wa shirika la chakula duniani(WFP) Saidi Johari alisema kuwa pamoja na kuwa na mikakati ya kusambaza vyakula vyenye virutubisho vinavyotakiwa, lakini tatizo la utapiamlo bado limeendelea kuwaandama wakimbizi wengi.

Pamoja na kuwa tatizo la kudumaa kutajwa kuwa kubwa katika kambi ya wakimbizi,lakini hata hivyo takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoko Kusin mwa Jangwa la Sahara ambayo inakabiliwa kwa kiwango kikubwa na tatizo la utapiamlo.

Kulingana na takwimu hizo, zaidi ya asilimia 42 ya watoto wanaozaliwa nchini Tanzania wanakabiliwa na tatizo la kudumuu huku wengi wao wakiwa ni wale wenye umri wa chini ya miaka 5.