Ban alaani mashambulio Nigeria, ataka pande zinazopingana kutafuta suluhu kwa njia ya amani

13 Agosti 2013

Vikundi vyote vyenye msimamo mkali nchini Nigeria viache mashambulio yao dhidi ya raia wasio na hatia, ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika salamu zake za rambirambi kufuatia mashambulio yaliyosababisha vifo vya watu kwenye maeneo ya Mafa na Kondugo kwenye jimbo la Borno nchini Nigeria. Mashambulio hayo ya hivi karibuni yalisababisha vifo vya makumi kadhaa ya waumini ambao walipigwa risasi wakati wakiwa wanaswali kwenye msikiti. Katibu Mkuu amerejelea msimamo wake ya kwamba hakuna lengo lolote linaloweza kutimizwa kupitia ghasia. Badala yake ametaka pande zote husika kumaliza tofauti zao kwa njia za amani ikiwemo mashauriano.