Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu zaidi waendelea kukimbia makwao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Watu zaidi waendelea kukimbia makwao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Karibu wakimbizi 63,000 kutoka Jamhuri ya Afrika ya kati wamekimbilia mataifa jirani tangu kuanza kwa mzozo wa kisiasa nchi humo mwezi Disemba mwaka uliopita kwa mujibu wa Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR.Wakimbizi 40,500 wamekimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huku wengine 13,000 wakiingia nchiniChad. Taarifa Zaidi na Alice Kariuki.

 (Taarifa ya Alice Kariuki)

UNHCR inasema kuwa ina wasiwasi kuhusiana na jinsi hali ilivyo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati huku kukiripotiwa hali mbaya ya usalama kwenye maeneo mengi. Kwenye mji mkuu Bangui usalama kwa watoa huduma za kibinadamu ni njambo linalotia wasi wasi baada ya wafanyikazi wawili wa Umoja wa Mataifa kushambuliwa na kujeruhiwa vibaya na watu waaliokuwa na silaha wanaohusiana na kundi la waasi la Seleka. Adrian Adwards kutoka UNHCR anasema kuwa  watu wanazidi kuhama ndani mwa nchi ambapo hadi sasa watu 206,000 wamehama makwao.

"Kwenye maeneo ya vijijini hofu inaripotiwa kutanda miongoni mwa raia ambao kwa sasa wanabuni makundi ya kujilinda. Makabiliano kati ya wenyeji na wanachama wa kundi la Seleka yalitokea jana asubuhi na siku iliyotangulia kwenye kijiji cha Beboura kilicho umbali wa kilomita 30 kutoka mji wa Paoua karibu na mpaka na Chad. UNHCR kwa mara nyingine inatoa wito kwa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kufanya jitihada kuhakishia watu usalama na mali zao kote nchini ili kuzuia kuhama kwa watu na mateso."