UM wazindua utafiti kuhusu watu walemavu katika maeneo ya majanga

12 Agosti 2013

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na udhibiti wa hatari za majanga, UNISDR na wadau wake, leo wamezindua utafiti wa kwanza kabisa wa aina yake kuhusu watu wanaoishi na ulemavu, na uwezo wao wa kukabiliana na majanga.

Mkuu wa ofisi ya UNISDR, Margareta Wahlström, amesema utafiti huo utaangazia suala lililopuuzwa katika udhibiti wa majanga, ambalo ni mahitaji ya takriban watu bilioni moja au zaidi wanaokadiriwa kuishi na ulemavu. Bi Wahlström amesema, watu wapatao milioni 30 huathiriwa kila mwaka na majanga kama vile matetemeko ya ardhi na mengineyo yanayohusiana na hali ya hewa.

Utafiti huo ambao utaendeshwa kwenye tovuti ya intaneti, unauliza maswali kama vile: “Je, una mpango wa maandalizi yako binafsi kukabiliana na majanga?”

Unaangazia pia masuala ya uwezo wa kujilinda kutokana na tukio la janga, na kuwa na muda wa kutosha wa kukimbilia eneo salama kabla ya janga kutokea. Maswali mengine yanahusu ufahamu, ujuzi na ushiriki katika kudhibiti majanga kwenye ngazi za kitaifa na mikoani.

Matokeo ya utafiti huo yatatangazwa kwenye Siku ya Kimataifa ya Udhibiti wa Majanga, Oktoba 13.