Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhuru wa kujumuika nchini Uganda ulindwe: wataalam wa UM

Uhuru wa kujumuika nchini Uganda ulindwe: wataalam wa UM

Wataalam watatu huru wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa wameelezea kusikitishwa na kupitishwa kwa mswada wa sheria ya kudhibiti mikutano ya hadhara nchini Uganda, ambayo inapinga mikutano ya watu zaidi ya watatu bila idhini ya polisi, na ambayo pia inawapa mamlaka polisi kutumia bunduki wanaposimamia maandamano. Wataalam hao maalum, akiwemo mtaalam kuhusu uhuru wa kujumuika, yule anayehusika na watetezi wa haki za binadamu na yule wa haki ya kujieleza, wametoa wito kwa Uganda ifanyie marekebisho sheria hiyo ilopitishwa Agosti 6 2013, na kuunda sheria inayoenda sambamba na majukumu ya Uganda ya kimataifa kuhusu haki za binadamu. Mtaalam kuhusu hali ya watetezi wa haki za binadamu, Margaret Sekaggya, amesema vitisho vya polisi havina nafasi katika jamii ya uhuru, uwazi na demokrasia, na kuongeza kuwa matumizi ya silaha ni lazima yadhibitiwe ipasavyo. Naye mtaalam kuhusu uhuru wa mikusanyiko ya amani, Maina Kiai, amesema sheria ya kutaka watu kuomba idhini ya kukutana kutoka kwa mamlaka huenda kukeleta kupigwa marufuku kwa mikusanyiko fulani, na hivyo kukiuka majukumu ya Uganda ya kimataifa. Frank La Rue, mtaalam kuhusu haki ya kujieleza amesema kwa kuwataka watu kutotoa matamshi yoyote yanayokiuka sheria, sheria hiyo inaacha nafasi ya kubana ukosoaji wa serikali, na hivyo kukiuka uongozi wa kisheria.