Marekani yaipiga jeki IOM ili kutekeleza mpango wa kuwakwamua wahamiaji Zimbabwe

9 Agosti 2013

Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM nchini Zimbabwe limepokea kiasi cha dola za Marekani 750,000 ili kutekeleza majukumu yake ikiwemo yale yanayohusika na hali ya ubinadamu pamoja na kulinda ustawi wa makundi ya wahamiaji. Fedha hizo zilizotolewa na serikali ya Marekani kupitia idara yake ya usaidizi wa majanga kwa nchi za nje zitasaidia kuwakimu makundi ya watu waliokwenda uhamishoni lakini sasa wameamua kurejea nyumbani Zimbabwe na wale wanaoomba hifadhi ya muda. Ama kiasi hicho cha fedha kitawezesha kutekelezwa kwa mpango wa utoaji mafunzo ya ujengeaji uwezo wa kukabiliana na majanga ya dharura ikiwemo pia wimbi kubwa la wahamiaji nchini humo. Kwa hivi kumekuwa na mpango wa ushirikiano baina ya serikali ya Zimbabwe na IOM mpango ambao unalenga kukabiliana na tatizo la uhamiaji.