Walioathirika afya ya akili kutokana na kiwewe au kufiwa sasa kupata tiba: WHO

7 Agosti 2013

Shirika la afya duniani WHO hii leo limetoa mwongozo mpya wa tiba dhidi ya watu waliokumbwa na athari ya afya ya akili kutokana na kiwewe au wanapopoteza wapendwa wao. “Tumechukua uamuzi huu baada ya kupokea maombi lukuki kutoka kwa watoa tiba ya maradhi ya akili kwa watu waliokumbwa na madhila hayo”, ni kauli ya Dokta Oleg Chestnov ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa WHO Idara ya magonjwa yasiyo ya kuambukika. WHO inasema matukio yanayosababisha kiwewekamavile kushuhudia ghasia, vipigo au kupoteza jamaa hutokea katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Mathalani asilimia 10 ya washiriki wa tafiti za WHO katika nchi 21 walikiri kushuhudia ghasia, asilimia 21.8 walikumbwa na mizozo na wenzao huku asilimia 17 nukta Saba wakishuhudia ajali. Tafiti hizo kwa ujumla zimedhihirisha kuwa asilimia Tatu nukta Sita ya watu wote duniani wamekumbwa na athari za akili baada ya kupata kiwewe kutokana na matukio mbali mbali. Kwa mantiki hiyo WHO inasema kuwa mwongozo huo mpya sasa utatoa mwelekeo sahihi wa tiba anayopaswa kupatiwa mtu aliyeathirika kiakili baada ya kukumbwa na kiwewe au kupoteza jamaa wa karibu. Mwongozo huo unatarjiwa kuwa wa msaada pia kwa wahudumu wa afya ya msingi kwenye kambi za wakimbizi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter