Wataalam wa haki za binadamu wapaazia sauti hali CAR

5 Agosti 2013

Kundi la wataalam huru wa Umoja wa Mataifa, leo limepazia sauti hali ya haki za binadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, likionya kuwa utawala wa kisheria ni kama haupo, na kwamba utumiaji vibaya mamlaka na kutowajibika ni jambo la kawaida nchini humo.Wataalam hao wametoa wito kwa mamlaka za mpito nchini humo kuchukua hatua mara moja kukomesha ukiukwaji wa haki za binadamu na kuhakikisha wale wanaoutekeleza wanawajibishwa kisheria.

Wataalam hao ambao ni Christof Heyns, ambaye anahusika na mauaji kinyume na sheria, Juan E. Méndez anayehusika na utesaji na adhabu zinazokiuka utu, na mtaalam kuhusu ukatili dhidi ya wanawake, Rashida Manjoo, wameelezea kusikitishwa na habari za mauaji, utesaji, watu kuzuiliwa rumande kiholela, ukatili wa kingono, kuwalazimu watu kutoweka, mazingira ya ukosefu wa usalama na kutokuwepo utawala wa kisheria, ambako kumeenea nchini humo kwa miezi mitano ilopita.

Mnamo mwezi Machi 2013, waasi wa Seleka waliitimua serikali ilokuwepo mamlakani, na sasa taifahilolinaongozwa na mamlaka ya baraza la mpito, likiongozwa na Michel Djotodia.