Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awasihi watu wa Zimbabwe wadumishe amani baada ya uchaguzi

Ban awasihi watu wa Zimbabwe wadumishe amani baada ya uchaguzi

  

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema amekuwa akifuatilia harakati za uchaguzi nchini Zimbabwe kwa karibu, na kuwapongeza watu wa taifa hilo kwa kudumisha amani kwenye siku ya uchaguzi na kwa kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.

Wakati huo huo, amesisitiza kuwa manung’uniko yaliyojitokeza kutokana na jinsi uchaguzi huo ulivyoendeshwa yanatakiwa kushughulikiwa kupitia utaratibu uliowekwa. Amesema manung’uniko hayo yanatakiwa kutizamwa kwa njia ya uwazi na haki, na kwamba muhimu zaidi ni kwamba matakwa ya watu wa Zimbabwe yaheshimiwe.

Katibu Mkuu anataraji kuwa mazingira ya utulivu na amani ambayo yamekuwepo wakati wa kupiga kura yataendelezwa wakati wa kuhesabu kura, hadi harakati nzima za uchaguzi kumalizika.

Amerejelea ahadi zilizotolewa na rais wa sasa na Waziri Mkuu na vyama vingine vya kisiasa kuhakikisha uchaguzi wenye amani, na kuwataka watoe ujumbe dhahiri wa kuwatuliza wafuasi wao. Umoja wa Mataifa unatoa wito uwepo uongozi wa kuwajibika na kuwajumuisha wote nchini Zimbabwe, pamoja na sera na marekebisho ambayo yataimarisha demokrasia na kujikwamua kiuchumi.