Taasisi za dola Jamhuri ya AFrika ya kati zaporomoka

2 Agosti 2013

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati inaelezwa kuwa taasisi za dola ziko mbioni kuporomoka na mamlaka thabiti ya dola kudorora. Hayo ni kwa mujibu wa Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu, Ivan Šimonović. George Njogopa anaripoti. (TAARIFA YA GEORGE NJOGOPA)

Šimonović amesema kuwa mamlaka  nyingi za kidola hazipo katika maeneo yaliyoko nje ya Mji Mkuu Bangui hatua ambayo inatoa picha halisi ya kuanguka kwa taasisi hizo.

Mamlaka hizo ni pamoja na kukosekana kwa utawala wa kisheria, kutokuwepo kwa polisi na mifumo mingine ya ufuatiliaji wa huduma za kijamii. Wananchi kwenye maeneo hayo wanaishi katika hali ya hofu na wasiwasi mkubwa.

Miongo kadhaa ya mapigano pamoja na kukosekana kwa utengamano wa kisiasa kumesababisha mifumo mingi ya utoaji haki na huduma za kijamii kuvurugika.

Vyombo kama mahakama na mihimili mingine ya kidola imeondoka kabisa na hivyo kuweka mazingira magumu kwa taifahilokuendesha uchaguzi huru na wa haki.

Mtalaamu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa,serikali ya mpito iliyoundwa hivi karibuni imeendelea kuzorota jambo ambalo halitoi matumaini mema kwa mustakabali wa taifa. Ametoa matamshi hayo kufuatia ziara yake ya siku nne nchini humo.