Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Unyonyeshaji ndiyo njia ya bora zaidi ya kuokoa maisha ya mtoto:UNICEF

Unyonyeshaji ndiyo njia ya bora zaidi ya kuokoa maisha ya mtoto:UNICEF

Huku wiki ya unyonyeshaji ikingo’a nanga hii leo Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF linalichukua suala ya unyonyeshaji watoto kama moja ya njia bora zaidi ya kuokoa maisha ya mtoto. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya (Taarifa ya Grace)

Watoto wanaonyonyeshwa ipasavyo wana uwezo wa kuishi mara 14 zaidi katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya maisha yao kuliko wale ambao hawakunyonyeshwa. Kumyonyesha mtoto siku ya kwanza baada ya kuzaliwa kunaweza kupunguza hatari ya kufa kwa mtoto kwa hadi asilimia 45.

Mkurugenzi mkuu wa UNICEF Geeta Rao Gupta anasema kuwa hakuna njia yoyote ya kuboresha afya ya mtoto kama kumyonyesha , njia ambayo ina gharama ya chini akiongeza kuwa unyonyeshaji ndiyo chanjo ya kwanza kwa mtoto.

Kumnyonysha mtoto pia humfanya kuwa wa haraka kujifunza na pia huzuia uzito wa juu kwa mtoto na magojwa yasiyo na tiba baadaye maishani.Utafiti wa hivi majuzi nchini Marekani na Uingereza unaonyesha kuwa watoto walionyonyeshwa hawapatwi na magonjwa kwa urahisi.

Kando na manufaa kwa watoto pia akina mama wanaonyonyesha huwa wanajiepusha kuwa wajawazito kwa kipindi cha miezi sita ya kwanza na mwili kurudia hali yake ya kawaida kwa haraka na pia huwa wanaepukana hatari ya ugonjwa wa saratani ya matiti baadaye maishani.