UNICEF yataka kuchukuliwa hatua za dharura kupambana na dhuluma dhidi ya watoto

31 Julai 2013

Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa linasema kuwa dhuluma kwa watoto mara nyingi hazitambuliwi wala kuripotiwa ambapo limetangaza mpango ambao unawataka wananchi wa kawaida, watunza sheria na serikali kuchukua hatua madhubuti kupambana na dhuluma za watoto.Jason Nyakundi na taarifa kamili.

(Taarifa ya Jason)

Mpango huu unajiri baada ya dhuluma ambazo zimetendewa watoto zikiwemo za mwezi Oktoba mwaka 2012 ambapo Malala Yousafzai mtoto mwenye umri wa miaka 14 raia wa Pakistan alipigwa risasi pamoja na mauaji ya watoto 26 na walimu kwenye eneo la Newtown Connecticut nchini Marekani mwezi Disemba mwaka 2012 na pia misururu ya visa vya kubakwa kwa wasichana nchini India na Afrika Kusini mwaka 2013. Mkurugenzi mkuu wa UNICEF Antony Lake anasema kuwa kwa kila nchi na kila tamaduni kuna dhuluma dhidi ya watoto akiongeza kuwa hatua zinastahili kuchukuliwa. Mpango huo ulizinduliwa kwa njia ya Video iliyozimuliwa na balozi mwema wa UNICEF Liam Neeson ambaye anaongoza kampeni za kupambana na dhuluma dhidi ya watoto. Watoto wasichana milioni 150 na wavulana milioni 73 walio chini ya miaka 18 wamedhulumiwa kimapenzi kulingana na Shirika la afya duniani WHO huku wengine milioni 1.2 wakisafirishea kiharamu kila mwaka kulingana na ripoti ya shirika la kazi duniani ya mwaka 2005.