Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israeli na Palestina zaanza mazungumzo jijini Washington DC

Israeli na Palestina zaanza mazungumzo jijini Washington DC

Pande nne katika mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati zimetoa taarifa ya pamoja za kuunga mkono tangazo la Marekani kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje John Kerry ya kwamba mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Israelna Palestina yameanza jana mjini WashingtonDCkuelekea awamu ya mwisho ya mashauriano.

Pande hizo ni Umoja wa Mataifa, Urusi, Marekani na Umoja wa Ulaya ambazo kwenye taarifa yao zimewasifu Kiongozi wa wapalestina Mahmoud Abbas na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa kuchukua uamuzi huo wa kijasiri kwa maslahi ya wananchi wao na kujizatiti kushirikiana na pande husika kufikia suluhisho la mataifa mawili ndani ya muda uliokubalika wa miezi Tisa.

Wamerejea taarifa za awali zinazotaka Palestina na Israel kuchukua kila hatua inayowezekana kuweka mazingira stahili ya kufanikisha mchakato wa mashauriano na kuepuka vitendo ambavyo vitaondoa kuaminiana.

Halikadhalika wametoa shukrani zao kwa Rais Barack Obama na Bwana Kerry kwa kusaidia pande mbili hizo kufikia makubaliano ya kuanza mazungumzo huku wakiusifu Umoja wa nchi za kiarabu kwa dhima yake thabiti ya kuwezesha kuanza tena kwa mashauriano hayo.