Baraza la Usalama laongeza muda wa ujumbe wake Côte d’Ivoire,Cyprus na Darfur

30 Julai 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limehitimisha kazi yake kwa mwezi Julai kwa kupiga kura ya kupitisha maazimio ya kuongeza muda wa huduma za ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Côted’Ivoire,Cyprus na eneo la Darfur, Sudan. Joshua Mmali na taarifa kamili(TAARIFA YA JOSHUA MMALI)

Baraza hilo limepiga kura, na kwa kauli moja, kuazimia kuongeza muda wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Darfur, UNAMID, kwa miezi 13 zaidi, hadi Agosti 31 mwaka 2014. Baraza la Usalama pia limeomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa awasilishe mapendekezo kuhusu jinsi ya kuboresha utendaji kazi wa UNAMID kwa Barazahiloifikapo Februari mwakani.

Katika hatua nyingine, Baraza hilo kwa kauli moja limepitisha azimio la kuongeza muda wa ujumbe wa  Umoja wa Mataifa nchini Cote d’Ivoire, hadi Juni 30 mwaka 2014, na kuamua kuwa ujumbe huo utakuwa na askari jeshi 7, 137.

Baraza hilo pia limepiga kura ya kuongeza muda wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Cyprus, UNFICYP, kwa kipindi cha miezi sita zaidi hadi Januari 31 mwakani, na kuunga mkono kuanza kwa mazungumzo mapema baina ya pande zote za kisiasa nchini humo.Azerbaijan na Pakistan hazikushiriki kura hiyo.