Ban atiwa wasiwasi na kuzorota hali ya usalama Iraq

29 Julai 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameelezea hofu yake kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama nchiniIraq, na kulaani vikali vitendo vya kigaidi na ghasia za kidini ambazo zinalenga kusambaratisha mfumo wa kijamii wa nchi hiyo.

Amesema ripoti za mauaji ya watu wapatao 50 hii leo katika mashambulizi ya mabomu ya magari kwenye maeneo yanayokaliwa na WaShia ni tukio la karibuni zaidi la machafuko ambayo sasa yamekuwa jambo la kawaida.

Katika taarifa ilotolewa na msemaji wake, Katibu Mkuu ametuma risala za rambirambi kwa familia za wahanga na serikali yaIraq, na kuwatakia majeruhi wote nafuu haraka. Ametoa wito kwa mamlaka zaIraqkuwafikisha walotekeleza mashambulizi hayo mbele ya sheria.

Bwana Ban amesemaIraqipo kwenye njia panda, na viongozi wake wa kisiasa wana wajibu wa kuirejesha nchi hiyo kutoka kwenye hali ya machafuko na kuhakikisha hawatoi nafasi kwa wale ambao wanataka kudakia mkwamo wa kisiasa na kueneza ghasia na ugaidi.