Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandalizi ya uchaguzi Mali yalikuwa mazuri licha ya changamoto Kaskazini: Afisa UM

Maandalizi ya uchaguzi Mali yalikuwa mazuri licha ya changamoto Kaskazini: Afisa UM

Wakati wananchi wa Mali wamehitimisha mchakato wa upigaji kura kwenye uchaguzi wa Rais, Naibu Mkurugenzi kutoka kitengo cha usaidizi wa upigaji kura cha Umoja wa Mataifa Ali Diabacté amesema zoezi hilo limefanyika kwa amani na maandalizi yalikuwa mazuri licha ya kwamba waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni wengi maeneo ya Kusini mwa Mali kuliko Kaskazini.Bwana Diabacte ambaye yuko Bamako kusaidiana na UNDP na ofisi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA kwenye mchakato huo wa uchaguzi amesema tofauti hiyo inatokana na kwamba maandalizi yalichelewa ikiwemo baadhi ya watu kutoona majina yao akitolea mfano wa eneo la Kidal.

Huko Kidal, kutokana na kwamba kulikuwa na mashauriano, maandalizi hayakufanyika kwa wakati, watu hawakuweza kupiga kura kama maeneo mengine ya Timbuktu na Gao. Watu  hawakuweza kuona majina yao, hawakuweza kuona shahada zao, hakukuwa na maandalizi mazuri, ijapokuwa kule ambako vituo vya kupiga kura vilikuwa wazi, waliweza kupiga kura. Lakini kusini hususan eneo la Gao nilikuwepo mwenyewe na niliona wengi walijitokeza kupiga kura bila tatizo lolote la usalama, maandalizi yalikuwa mazuri. Ijapokuwa katika maeneo mawili vituo viwili havikufunguliwa kwani walikuwa wanahofia kikundi cha NMLA na hivyo walilazimika kuvifunga.”