Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi Mali ufanyike kwa amani: Ban

Uchaguzi Mali ufanyike kwa amani: Ban

Wakati Mali inajiandaa kufanya uchaguzi wa Rais jumapili tarehe 28 mwezi huu, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa wito uchaguzi huo ufanyike kwa amani na uwazi. Bwana Ban ametaka pande zote husika kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa kuzingatia kanuni huku akiwasihi wapiga kura nchini humo kutekeleza haki yao ya kidemokrasia ya kupiga kura.

Halikadhalika ameunga mkono mwongozo wa utendaji ulioridhiwa na wagombea akisema ni matumaini yake kuwa watauzingatia ikiwemo kuhakikisha utata wowote unaojitokeza unapatiwa suluhu kwa amani na sheria. Bwana Ban amesema uchaguzi wa Mali ni muhimu katika kurejesha utawala wa kikatiba, mashauriano na maridhiano ya kitaifa huku akisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia mchakato wa amani na utulivu nchini Mali.