Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili Iraq, Somalia na kusikiliza ripoti kuhusu Darfur

Baraza la Usalama lajadili Iraq, Somalia na kusikiliza ripoti kuhusu Darfur

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadili masuala kadhaa, yakiwemo Iraq, Somalia na mzozo wa Darfur nchini Sudan, ambapo limesikiliza pia ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu ujumbe wa pamoja wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa katika eneo la Darfur. Flora Nducha ana maelezo zaidi

TAARIFA YA FLORA NDUCHA

Akiwakilisha ripoti ya Katibu Mkuu, Mwakilishi wake ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa pamoja wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa Darfur, UNAMID, Mohammad Ibn Chambas, ameliambia Baraza la Usalama kuwa suluhu la kisiasa kwa mzozo wa Darfur ndiyo njia pekee endelevu kwa pande zote zinazozozania eneo hilo.

Bwana Chambas amesema kuandama malengo ya kisiasa kwa njia ya vita kwa mwongo mmoja ulopita kumechangia tu maafa ya muda mrefu kwa watu wa Darfur. Amerejelea mwito wake kwa serikali ya Sudan na makundi yenye silaha ambayo hayajatia saini makubaliano ya amani kusitisha mara moja mapigano, na kujielekeza kwenye meza ya mazungumzo ya amani bila masharti.

Tangu mwanzoni mwa mwaka, mapigano kati ya serikali ya Sudan na makundi yenye silaha, yamesababisha, siyo tu raia kupoteza maisha, bali pia hali ya kuwalazimu watu kuhama makwao na kusambaritisha shughuli zao za kijamii na kiuchumi na uharibifu wa mali. Raia hao hawaonekani kama wamelengwa maksudi, lakini athari kubwa kwao bado ni kulazimika kuhama, majeraha na vifo.

Ripoti hiyo ya Katibu Mkuu pia imelaani vikali mashambulizi manne tofauti dhidi ya vikosi vya kulinda amani vya UNAMID, likiwemo lile Julai 13, ambalo lilisababisha vifo vya walinda amani saba wa Tanzania, na kuwajeruhi wafanyakazi wengine 17 wa UNAMID.

Baraza la Usalama pia, limepitisha maazimio mawili mapema leo asubuhi, moja kuhusu Iraq na jingine kuhusu Somalia.